Tanzania emblem

Tanzania Fertilizer Regulatory Authority

News

Tanzania kuadhimisha Siku ya Mbolea Duniani Oktoba 13, 2020


Tanzania itaungana na nchi nyingine dunianikuadhimisha Siku ya Mbolea Duniani ambayo kila mwaka hufanyika tarehe 13 Oktoba.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt.Stephan Ngailo amesema maadhimisho hayo hapa nchini yatafanyika katika Kijiji cha Dakawa kilichoko Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro.

Dkt.Ngailo amesema lengo la maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani ni kupata wigo mpana zaidi wa kuelezea masuala mbalimbali katika tasnia ya mbolea ikiwemo mafanikio ya tasnia ya mbolea nchini, kutoa elimu kwa wadau wa mbolea hususan wakulima na wafanyabiashara wa mbolea ili waweze kujua mifumo mbalimbali ya upatikanaji na usambazaji wa mbolea.

Amesema siku hiyo pia hutumika kutoa elimu kuhusu namna TFRA inavyosimamia ubora na biashara ya mbolea ili kuwahakikishia wakulima wadogo upatikanaji wa mbolea bora kwa wakati, kwa bei nafuu na kwa msharti rafiki ya ulipaji.

Lengo la uelimishaji huu Dkt. Ngailo amesema ni kuwapa wadau uelewa mpana na hivyo kuwawezesha kuona fursa zilizopo na kuzitumia katika kuongeza tija ya uzalishaji kwa ajili ya kutosheleza mahitaji ya chakula na malighafi ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Dkt. Ngailo ameongeza kuwa katika siku hiyo wadau mbalimbali kutoka taasisi za utafiti, vyuo vikuu na asasi zisizo za kiserikali watapata fursa ya kutoa elimu kwa wakulima ikiwemo matumizi sahihi ya mbolea na afya ya udongo.

Makampuni yanayozalisha, kuingiza na kusambaza mbolea nchini yataonesha aina mbalimbali za mbolea wanazozalisha ili kutoa uelewa mpana kwa wakulima kuhusu matumizi sahihi ya mbolea hizo. Makampuni hayo ni pamoja na Afrisian Ginning Ltd, Sianga Intertrade Company Ltd, Guavay Fertilizer Company Ltd, Keenfeeders Ltd, Dodoma Cement, ABM Equipment and Service Ltd na ETG inputs.

Zao la Mpunga uliostawi na kuzaa vizuri baada ya kutumia mbolea kwa usahihi

Zao la Mpunga uliostawi na kuzaa vizuri baada ya kutumia mbolea kwa usahihi


Makampuni mengine yaliyothibitisha kushiriki katika maadhimisho hayo ni Minjingu Minies and Fertilizer Ltd, PremiumAgrochem Ltd, HAPCO Agro Business, Isacha Feeder Intertrade Company, Mtali Agrotrader Company na FarmTimes Company& Farm Products.

Kaulimbiu katika maadhimisho hayo, Dkt.Ngailo amesema ni “Kuwawezesha Wakulima Wadogo Kupata Mbolea Bora, KwaWakati na kwa Bei Nafuu”.

Amesema maadhimisho hayo yatajumuisha zaidi ya washiriki mia nne (400) kutoka ndani na nje ya mkoa wa Morogoro. Mgeni rasmi atakuwa ni Waziri Wa Kilimo Mhe. Japhet Ngailonga Hasunga.

Siku ya Mbolea Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 13 Oktoba ikiwa ni kumbukizi ya uvumbuzi wa kirutubishi aina ya amonia kinachopatikana hewani, uvumbuzi huu uliofanywa na Bwana Fritz Haber mwaka 1908 mwanasayansi kutoka nchini Uingereza.

Siku hii iliadhimishwa kwa mara ya kwanza tarehe 13 Oktoba 2016 nchini Uingereza. Kuadhimishwa kwa siku hii ni mpango wa Kimataifa unaoungwa mkono na Jumuiya za Sekta ya Mbolea duniani kwa lengo la kuelimisha umma kuhusu faida na matumizi ya mbolea na kutia moyo Juhudi za ubunifu katika teknolojia za mbolea katika Kilimo kwa mustakabali wa maendeleo endelevu.

Uvumbuzi huu ulichochea mapinduzi ya kijani katika karne ya 20 yaliyowezesha kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao kutokana na matumizi ya mbolea yaliyosaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa janga la njaa na kuleta uhakika wa chakula katika nchi nyingi duniani.

Utumiaji wa mbolea kwa usahihi huongeza tija katika uzalishaji wa mahindi.

Utumiaji wa mbolea kwa usahihi huongeza tija katika uzalishaji wa mahindi.

Zao la biashara la Tumbaku lililostawi vizuri baada ya kutumia mbolea

Zao la biashara la Tumbaku lililostawi vizuri baada ya kutumia mbolea